Home » » Tanzania yapata ufadhili uboreshaji wa bandari, reli

Tanzania yapata ufadhili uboreshaji wa bandari, reli

Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
 
Tanzania imepata bahati ya kufadhiliwa kwa mradi wa ukanda wa uchukuzi wa kati wenye Bandari Kuu kutoka Dar es Salaam, hadi nchi za Kaskazini Magharibi mwa nchi, utakajikita kwenye uboreshaji wa bandari na miundombinu ya reli ya kati.
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema mradi huo ni kati ya miradi 35 iliyowasilishwa na nchi mbalimbali duniani mbele ya jopo la wataalamu katika mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Uchumi uliofanyika Januari mwaka huu  nchini Uswisi.

Alisema katika mkutano huo, nchi mbalimbali ziliwasilisha miradi yenye kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwenye nchi za Afrika.

Alisema miradi 16 ilionekana ni yenye kikidhi vigezo na kati yake mradi huo ulionekana ni bora na utaleta matokeo chanya kwa maendeleo ya nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Alisema sifa zilizosababisha mradi wa Tanzania kuonekana unaofaa ni mikakati mizuri iliyoanishwa chini ya mpango wa Matokeo Makubwa Sasa kufanya sekta ya uchukuzi kuleta mabadiliko kwenye uchumi na ushiriki wa sekta binafsi katika kuboresha miundombinu.

Alisema amemuonba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuunda kamati ndogo ya kitaifa ya kusimamia mradi huo ambao unategemewa kuivusha nchi kutoka kutegemea usafiri wa barabara kwenye mizigo kutoka bandarini na kuwa usafiri wa reli ambao ni rahisi na hauna gharama kubwa.

Wajumbe wa kamati hiyo ni kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Mamlaka ya Bandari (TPA); Kampuni Hodhi ya Rasilimali ya reli (Rahco); Shirika la Reli Tanzania (TRL), Wizara ya Fedha, Wizara ya Uchukuzi na Tume ya Mipango.

Alisema fedha za utekelezaji wa mradi huo zitatokana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (Badea) na wahisani wengine.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa