Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wanawake nchini wameaswa kujenga tabia ya kutunza akiba, ili kufikia malengo wanayojiwekea kwa maendeleo ya familia zao.
Akifungua tamasha la kwanza la wanawake na vijana
lililopewa jina la Mwanamke na Akiba mwishoni mwa wiki iliyopita, Mke wa
Makamu wa Rais, Asha Bilal alisema tamasha hilo ni fursa ya kupata
utaalamu na kupanua wigo wa biashara.
Bilal alisema maendeleo ya Tanzania yanaanza kwa mwanamke kujijengea tabia ya kujiwekea akiba, ambayo ni mkombozi wa baadaye.
“Akiba ni msingi wa maendeleo ya kila mwananchi.
Kwa biashara na kila ajira tuliyonayo, bila kuwa na elimu na utaratibu
wa kujiwekea akiba tutazidi kuwa na kipato kidogo hivyo kushindwa
kujikwamua na umaskini,” alisema Bilal.
Alipongeza Kampuni ya Angels Moment na timu yake
kwa kuandaa tamasha hilo la elimu kwa wanawake, hususan waliopo sekta
isiyo rasmi kwani linatoa nafasi ya kuwaondoa kwenye utegemezi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Angels Moment,
Naima Malima alisema lengo la tamasha hilo ni kuboresha kasumba ya
kujiwekea akiba.
“Tamasha hili limeandaliwa kuwaonyesha wanawake na
vijana umuhimu wa kuweka akiba, aina tofauti za kuweka akiba na njia
mbalimbali za kuweka akiba na fursa kupitia uwasilishaji mada na
maonyesho,” alisema Malima. Alisema washiriki watapata fursa ya kupata
elimu kuhusu kukabiliana na hatari ya uhifadhi wa fedha, masuala
mbalimbali yanayohusu usimamizi wa fedha.
“Tamasha linatoa fursa za maonyesho na semina
ambazo zitawaelimisha wanawake namna tofauti za kuweka akiba, na mbinu
mbalimbali za kujikimu,” alisema Bi Naima.
Aliongeza kuwa Tamasha hili pia linakusudia
kuwaelimisha wanawake umuhimu wa kuweka akiba, mbinu tofauti za kuweka
akiba na jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika kujiwekea
akiba.
Tamasha hilo linalofanyika katika Ukumbi wa Dar
Live - Mbagala, jijini Dar es Salaam limehudhuriwa na mamia ya kina mama
na vijana ikiwemo wake wa viongozi waliongozwa na Mama Tunu Pinda
ambaye ameshiriki kama mjasiriamali wa kuuza mazao ya nyuki.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment