Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal amekitaka Chama cha
Hisabati Tanzania (Chahita) na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kukaa
meza moja ili kuondoa tofauti zilizopo kuhusu namna ya wanafunzi wa
darasa la saba kufanya mtihani wa hisabati.
Uamuzi huo umekuja baada ya Necta kuanzisha mfumo
wa maswali ya kuchagua katika mtihani wa hisabati, tofauti na ilivyokuwa
awali ambapo mwanafunzi alikuwa akikokotoa hesabu hizo. Chahita
wanapinga mfumo mpya.
Akizungumza katika maadhimisho ya sherehe ya miaka
kumi ya Siku ya Pai (3.14) Tanzania iliyofanyika Dar es Salaam jana, Dk
Bilal alisema, wote wawili wanasababu za msingi, kinachotakiwa ni
kuangalia wapi kuna makosa.
“Najua ninyi wana mahesabu hampendi maswali ya
kuchagua na mna sababu zenu, Necta nao wanasababu zao, hivyo kaeni
pamoja mjadiliane ili kumaliza tofauti zilizopo kwa amani kabisa,”
alisema Dk Bilal.
Alisema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN)
unatakiwa kuonekana kwa vitendo na kwamba utaweza tu kufanikiwa iwapo
ushirikiano kati ya jamii na wadau utakuwapo na kuimarishwa kikamilifu.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa
Chahita, Dk. Sylvester Rugeihyamu alisema wanafunzi wanahitimu darasa la
saba na kujiunga na kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma, kuandika
na kuhesabu kwamba hayo ni matokeo ya kufanya mtihani wa hisabati kwa
mfumo wa kuchagua.
“Chama kilikataa mfumo huu wa kuchagua majibu tena
kwa somo la hisabati, haifai hata siku moja, hesabu lazima ukokotoe na
tunatakiwa kuwajenga wasomi wa nyanja hii sasa kwa njia hii hatuwezi
kuwapata,” alisisitiza Dk Rugeihyamu.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment