Home » » Matokeo Makubwa Sasa yamelenga kupunguza nakisi bajeti ya Serikali

Matokeo Makubwa Sasa yamelenga kupunguza nakisi bajeti ya Serikali

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Saada Mkuya, Waziri wa fedha
 
Utaratibu wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN)  ni kupunguza nakisi katika bajeti ya serikali kwa Sh. trilioni nne kufikia mwaka 2015/16.
 
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Utendaji katika Wizara ya Fedha, Emmanuel Tutuba, wakati akielezea kuhusu utaratibu wa wizara katika kutekeleza BRN.
 
Tutuba alisema malengo ya wizara yake ni pamoja na kupunguza nakisi ya bajeti na kutafuta mapato ya ziada kiasi cha Sh. Trilioni 3.8 kwa miaka hiyo.
 
Alisema lengo lingine ni kutekeleza miradi ya ushirika wa pamoja kati ya sekta binafsi na Umma (PPP).
 
Tutuba alisema serikali imelenga kushirikiana na sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya kimkakati yenye thamani ya Sh. Trilioni 6 hadi ifikapo mwaka 2015/16. Alisema miradi ya awali ambayo imebainishwa kuanza kutekelezwa kwa ubia huo ni ujenzi wa  barabara ya Dar es Salaam hadi Chalinze.
 
Miradi mingine ni uendeshaji wa mradi wa mabasi yaendayo haraka Dar es Salaam na ujenzi wa kituo cha kufua umeme cha kinyerezi 111. Pia alisema utekelezaji wa viashiria vya kudhibiti matumizi ya serikali utazingatiwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15 kama ilivyopangwa wakati wa uchaguzi wa kimaabara wa BRN.
 
Kuhusu kutoa fedha katika wizara zinazotekeleza BRN, alisema wizara yake itaendelea kutekeleza jukumu la kutafuta na kutoa fedha za kugharamia shughuli za utaratibu huo.
 
Alisema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba mwaka jana wizara yake ilitoa fedha za maendeleo kwenye wizara zinazotekeleza mradi huo. Alitaja miradi hiyo kuwa ni elimu ambayo ilipewa Sh. Bilioni 8.3, maji Sh. Bilioni 86.0, kilimo Sh. Bilioni 10.2, uchukuzi Sh. Bilioni 146.6 na nishati Sh. Bilioni 339.4.
 
Kadhalika alisema kati ya Julai/Disemba mwaka huo jumla ya Sh. Bilioni 10.9 zilikusanywa kutokana na utekelezaji wa hatua za BRM za kuongeza mapato yasiyo ya kodi.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa