Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JESHI
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limedai kubaini mbinu mpya za
kusafirisha dawa za kulevya kama cocaine, heroine.
Kamanda wa
Polisi wa kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova, aliyasema hayo Dar es
Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema jeshi
hilo limegundua mbinu hiyo baada ya kuwakamata watu wanne kati yao wapo
raia watatu wa Nigeria, mmoja Mtanzania, wanaojihusisha kusafirisha
dawa hizo.
"Watuhumiwa walikamatwa Machi 18 mwaka huu, katika Ofisi
za Kampuni ya DHL, Barabara ya Sam Nujoma, mkabala na Mlimani City,
Mwenge wakijiandaa kusafirisha dawa hizo katika kifurushi," alisema.
Aliwataja
watuhumiwa kuwa ni Sunday Chaidikaobi (42), Chukwuma Favour (31),
Franklin Indubuisi (41) ambao ni raia wa Nigeria na Hadija Ngoma (43),
Mtanzania na mkazi wa Kimara Temboni.
"Watu hawa walikutwa na
kifurushi kilichokuwa kikisafirishwa kwenda nchini Liberia, Afrika
Magharibi, upekuzi ulifanyika kwa umakini na kubainika kilikuwa na dawa
za kulevya.
"Kifurushi hicho kilikuwa na vitabu vitatu vya lugha ya
Kiingereza ambavyo katikati ya kurasa za mwanzo na mwisho kulikuwa na
unga wa rangi ya kahawia unaoashiria ni heroini," alisema.
Alisema
dawa hizo zinakadiriwa kuwa na ujazo wa nusu kilo na uchunguzi zaidi
unafanyika ili kubaini thamani, ujazo halisi na aina ya dawa ambapo
sampuri yake imepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi.
Wakati huo huo, jeshi hilo linawashikilia watu wawili wenye asili
ya Asia wakidaiwa kuhusika na tukio la kuwateka nyara watoto wawili wa
kike wa mfanyabiashara wa simu za mkononi katika Mtaa wa Samora, Dar es
Salaam, Bw. Aunally Jaffer.
Kamishna Kova, aliyasema hayo wakati
akizungumza na waandishi wa habari na kudai polisi walipata taarifa kuwa
kuna mpango wa kuwateka watoto hao Machi 14 mwaka huu.
Mpango huo
ulikuwa ufanywe na watuhumiwa Adil Yusuf (24), mkazi wa Kariakoo na
Mehul Kava (24), mkazi wa Mtaa wa Jamhuri na Zanaki.
"Lengo la
watuhumiwa ni kujipatia fedha sh. milioni 500 baada ya kufanikisha
utekaji huo kutoka kwa wazazi wa watoto hawa, ndugu na jamaa zao...hawa
watoto ni Shamima Aunally na Halifa Aunally wote wakazi wa Mtaa wa
Kisutu na Zanaki," alisema.
Aliongeza kuwa, makachero wa kanda hiyo
waliweka mtego na ilipofika Machi 14, saa nane mchana, watuhumiwa
walikamatwa wakiwa tayari kuwateka mabinti hao katika eneo la Jet Rumo,
Manispaa ya Ilala, kabla ya kutimiza lengo lao.
Kamishna Kova alisema, baada ya kuwahoji watuhumiwa wote walikiri na kudai lengo lilikuwa kupata sh. milioni 500.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment