Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » ABIRIA DALADALA HATARINI

ABIRIA DALADALA HATARINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani,Mohamed Mpinga
Usalama wa abiria wanaotumia usafiri wa daladala, pikipiki, maarufu kama “bodaboda” na Bajaj upo hatarini kutokana na madereva wake kunywa pombe kali zinazofungashwa kwenye pakiti wakati wakiendesha vyombo hivyo vya moto.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE jijini Dar es Salaam katika manispaa zake tatu za Kinondoni, Ilala na Temeke, umethibitisha kuwa madereva hao hulewa wakati wakiendesha vyombo hivyo.
Pombe hizo hupatikana kwa wingi kwenye maeneo ya vituo vya daladala wakati wa mchana na ni kawaida kwa madereva na makondakta wao kunywa wakiwa kazini. Wengi huwa na pakiti hizo mifukoni na wengine huchanganya na maji ya kunywa ya chupa.

Baadhi ya vituo ambavyo NIPASHE ilitembelea na kuthibitisha pasi na shaka yoyote kuwa kuna uuzaji wa pombe hizo ni pamoja na Makumbusho, Ubungo, Buguruni, Tandika, Temeke Veterinary, Magomeni, Kigogo, Mbagala Rangi Tatu, Tegeta, Kimara, Mbezi Mwisho, Tabata Bima, Vingunguti, Jet Rumo, Banana, Gongolamboto, Tazara, Mwananyamala Magengeni, Mwananyamala A, Kinondoni Manyanya  na Ilala Boma.

Pia NIPASHE ilishuhudia uuzwaji wa pombe hizi kwenye vituo vya Buguruni Shell, Rozana, Keko Chang’ombe, Sabasaba, Big Brother Manzese, Manzese Bakhresa, Argentina, Kagaera na Mwembechai  na maeneo mengine mengi kati ya vituo 76 ambavyo NIPASHE  ilitembelea katika  uchunguzi uliodumu kwa wiki tatu.

Uchunguzi huo unaonyesha kuwa asilimia kubwa ya vituo vya daladala, bodaboda na bajaji jijini vimekithiri kwa uuzwaji wa pombe hiyo nyakati za mchana.

Takwimu zilizotolewa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, zinaonyesha kuwa tangu Januari mwaka jana hadi Januari mwaka huu, madereva waliokamatwa wakiendesha magari wakiwa wamelewa jijini Dar es Salaam ni 3,748.

Kamanda Mpinga alisema ajali zilizotokea mwaka 2013/2014 kwa mkoa wa Dar es Salaam ni 5,052 kati ya hizo Kinondoni inaongoza kwa kupata ajali 2,140 sawa na asilimia 42.3, Ilala ajali 1,561 sawa na asilimia 30.8 na Temeke ajali 1,351 sawa na asilimia 26.7.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na NIPASHE walisema kuwa unywaji pombe wakati wakuendesha chombo cha moto unachangia ajali nyingi zisizo kuwa za lazima.

Hilda Mamulilo mkazi wa Temeke alisema: “Mimi naona madereva wengi ndio watumiaji pamoja na makondakta wao kitu ambacho kinachangia ajali nyingi zisizo kuwa za msingi, kwa hiyo serikali iweke sheria ambayo inakataza uuzwaji wa pombe mchana,”alisema Hilda.

Aliongeza kuwa kama serikali haitasimamia jambo hilo kwa makini kutakuwa na vilema wasiokuwa na idadi kutokana na uzembe wa watu wachache.
Masudi Ramadhani mkazi wa Ilala alieleza kuwa Manispaa ya Ilala imekuwa ikiacha watu wanavunja sheria huku wakipewa adhabu dogo.

“Viongozi wa Ilala wanatakiwa kutunga sheria itakayo kuwa mfano kwa wengine, haiwezakani ukakuta dereva na kondakta wakiwa wamelewa na wanatoa matusi yasiyo ya kawaida huku watu wanawaangalia tu,” alisema Masudi.

Alilitaka jeshi la polisi kuwafuatilia wanaoelewa mchana na kuwafunga miezi sita bila dhamana ili wenzao wanapoangaika kuwatoa wajue kuwa siyo jambo la mchezo.

Mkazi wa Kinondoni ambaye ni fundi wa magari, Danieli Noha, alisema: “Madereva hawajui athari za kuendesha gari ukiwa umelewa pamoja na kuwaumiza abiria hata wao wenyewe (madereva) wanajiatarishia maisha yao,”alisema Danieli.

Baadhi ya wauzaji wa pombe kali kwenye vipakiti kwenye maeneo hayo walisema wamekuwa wakifanya biashara hiyo kwa muda na wateja wao wakubwa ni madereva na makondakta wa daladala.

Lucy Joseph muuza maji na pombe hizo kwenye kituo cha daladala Tandika alisema:  “Mimi nauza viroba kwa muda mrefu kwa sababu mwanzo nilikuwa na uza maji pamoja na juisi lakini nilivyoona madereva na makondakta wanaulizia viroba sana nikaamua kuanza kuuza na kweli siyo haba kwa siku naweza kuuza viroba zaidi ya 20 ukichanganya na mauzo ya juisi na soda siyo haba watoto wanaenda shule,” alisema Lucy.

“Unajua kunywa pombe wakati wakazi siyo vizuri, lakini kwa vile watumiaji wanahitaji na mimi nahitaji fedha inanibidi niuze,” aliongeza.
Hemedi Mbonde muuzaji wa viroba eneo la Ubungo alisema:

“Siyo siri watumiaji wakubwa wa viroba ni waendesha bodaboda na daladala nakwambia kwa sasa hakuna mauzo ya pombe mengi kama viroba. Mimi nauza maji, lakini maji wananunua abiria wanaopita njia huiwezi kumkuta dereva wa bodaboda anatumia maji wengi wao ni viroba.

Wakizungumza na NIPASHE madereva na makondakta wa daladala walisema kunywa pombe na kusababisha ajali inategemea na dereva mwenyewe.

Mawazo Bakari dereva wa daladala inayofanya safari zake kati ya Makumbusho na Mbagala alisema: “Mimi nakunywa, lakini najielewa naendesha gari huu mwaka wa kumi sasa nimepata ajali mara mbili tu na ninalewa,”alisema Mawazo.

Aliongoza kusema hata kama hujalewa ajali utaipata tu, kwani zinasababishwa na barabara mbovu au matairi yanakuwa yameisha kwa hiyo lazima ajali itokee.

Issa Abdi dereva wa bodaboda alisema: “Nikweli ulevi ni hatari kwa afya yako hasa kipindi unachokuwa unaendesha gari au chombo chochote cha moto ila tunakunywa vile tumezoea ila nataka kuacha pombe niokoke.”

Alisema serikali inatakiwa kusimamia sheria ili kuhakikisha wanapunguza vifo vitokanavyo na ajali zinazosababishwa na madereva walevi.

Kondakta wa daladala, Learnld Mushi, alisema kuwa bila kupata pombe hafanyi kazi pombe ndiyo inamchangamsha na kumpa hari ya kufanya kazi.
Rama Mgosi dereva wa bajaji alisema ana uwezo wa kunywa pombe kwa siku nzima huku anaendesha bajaj yake, lakini anaamini inaweza kutokea akapata ajali.
“Pombe siyo nzuri ila tumezoea kwetu Tanga tunakunywa kabla ya kazi,”alisema Mgosi.Pamoja na Kamanda Mpinga kukiri kuwa tatizo la ulevi wa madereva ni kubwa, wamejipanga kupunguza hali hiyo.

Alisema sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 inakataza ulevi na kuendesha vyombo vya moto.“Tumejipanga kukabiliana tatizo hilo, kuanzia wiki ijayo tunaanza kutoa mafunzo kwa askari wa usalama barabarani namna ya kutumia vifaa maalumu vya kubaini madereva walevi,”alisema Mpinga.

Aliongeza baada ya kuanza mchakato huo na kubaini idadi ya watumiaji ikiwa kubwa wataomba kupigwa marufuku uzwaji wa pombe za viroba mchana.

Aidha Mpinga alifafanua kuwa kazi ya upimaji wa madereva walevi ilianza muda sasa kwa magari yaendayo mkoani ikiwemo malori na mabasi ya abiria, wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuwadhibiti madereva walevi.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Gunini Kamba, alithibitisha kuwapo kwa biashara ya pombe kali za vipakiti kwenye maeneo mbalimbali yasiyoruhusiwa kwa biashara hiyo vikiwamo vituo vya daladala.

Hata hivyo, alisema Manispaa haitoi leseni kwa wamachinga wanaofanya biashara maeneo yasiyo rasmi hasa kwenye vituo kama vya daladala.

“Ni kweli hali hiyo ipo sana nasi inatuumiza tunatuma askari wetu mara kwa mara wanawakamata, lakini hawasikii wamekuwa sugu. Embu fikiria mfanyabiashara anachukuliwa nakupigwa faini, lakini wapi anaendelea. Tunaomba polisi tusaidiane nao kwenye zoezi hili pamoja na ninyi waandishi wa habari,”alisema Gunini.

Msemaji wa Manispaa ya Temeke, Lilian Chawale, alisema hakuna anayeruhusiwa kufanya biashara kwenye maeneo yasio rasmi.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa