Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, akitoka kuhojiwa na Baraza la Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka, jijini Dar es Salaam jana.
Baraza la Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma, jana lililazimika kuahirisha shughuli zake baada ya kukosekana kwa vitabu vitakatifu kwa ajili ya walalamikiwa na walalamikaji kuapa kabla ya kutoa maelezo na ushahidi wao.
Licha ya Baraza hilo kuendelea na shughuli zake kwa kuwaapisha walalamikaji na walalamikiwa kwa kunyanyua mkono juu na kufuata maelezo ya mwongoza kiapo, lilishindwa kuendelea ilipo fika zamu ya Diwani wa Sinza.
Diwani huyo aliitwa mbele ya Baraza hilo baada ya Diwani wa Kata ya Kunduchi, Janeth Rite, kuapishwa kwa kutumia mkono. Lakini ilipo fika zamu ya diwani wa Sinza, Pamba Mkonga ambaye alikuwa amevalia fulana yenye maneno ya M4C (Movement for Change) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ilishindikana.
Baada ya kuapishwa kwa utaratibu wa kawaida, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Hamis Msumi, alihoji kama kiapo hicho ni halali kwa kuwa hakuna Biblia huku akiwahoji watumishi wa Sekretarieti sababu za kukosekana kwa vitabu hivyo.
”Kwanini hakuna Biblia wala Kur’an, hiki siyo kiapo, mmezipeleka wapi...siwezi kuwasubiri mkalete vitabu hivyo, ni vyema tuhairishe na wakati mwingine mje mkiwa mmejipanga ili mashahidi waape kwa mujibu wa vitabu vyao,” alisema Jaji Msumi.
Kutokana na hali hiyo, watumishi hao walionekana wakijitetea, lakini Jaji Msumi hakukubaliana nao na kuahirisha shauri hilo hadi leo, diwani huyo na walalamikiwa wengine watakapofika tena mbele ya Baraza hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Baraza, Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha Sekretarieti ya Maadili kwa viongozi wa umma, Philoteus Manula, alisema Baraza hilo linaendeshwa kwa kutumia busara na kwamba hakuna sheria inayolazimisha kuwepo kwa Biblia au Kur’an na kwamba mashauri yamekuwa yakiendeshwa bila vitabu hivyo.
Awali, Shahidi wa pili katika shauri la matumizi ya lugha za matusi na udhalilishaji wa watumishi na viongozi wengine dhidi ya Mkuu wa wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, amelieleza Baraza kuwa DC huyo ameandaa maandamano ya kumpokea.
Shahidi huyo, Hillary Ngonyani, ambaye ni diwani wa kata ya Kwamndolwa, alidai hayo jana mbele ya Jaji Msumi, wakati akiongozwa na mwanasheria Hassani Mayunga, kutoa ushahidi wake.
Alidai kuwa kiongozi huyo kutokana na majigambo, kutukana na kudhalilisha viongozi mbalimbali na kwamba leo baada ya kutoka kwenye shauri hilo kuna kundi la vijana wapiga debe wa kituo cha mabasi wameandaliwa kwa ajili ya kufanya maandamano ya kumpokea.
”Kiongozi huyu rafiki zake ni wapiga debe stendi, wavuta bangi, rafiki zake wamemuandalia maandamano ili ionekane Halmashauri ina makosa wakati shauri linaendelea...amekuwa akijitapa kuwa yeye ni mtoto wa Rais na hakuna mtu wa kumfanya lolote,” alidai.
Shahidi huyo alidai kuwa uongozi wake umejaa ubabe, jeuri, dharau na kiburi, na kwamba tatizo lilianza mwaka 2013, baada ya halmashauri kupokea fedha za ujenzi wa vyumba vya maabara kutoka Tamisemi zikiambatana na waraka maalumu wa maelekezo, lakini DC huyo alishinikiza kutumika mafundi wa kawaida.
Alidai Baraza la Madiwani liliitishwa na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji kutekeleza agizo la Tamisemi, lakini DC huyo akishirikiana na Katibu wa CCM wilaya, waliwaita Madiwani na kuwaonya juu ya agizo lao.
”Alitueleza tutake tusitake lazima agizo lake litimie, yeye ndiye serikali, kwa kuwa mmeamua kubishana na mimi sasa tutaenyeshana, kwa kuwa mmeamua kufanya kazi za serikali sasa tutaona nani zaidi kati ya nyinyi na mimi,” alidai Ngonyani.
Alidai baada ya hapo mkuu huyo wa wilaya alikataa wananchi kutochangishwa kwenye ujenzi wa maabara hizo, jambo ambalo liliifanya halmashauri kushindwa kutekeleza ujenzi wa chumba cha tatu cha maabara katika shule za sekondari za Nyerere na Mwombezi.
Ngonyani alidai kuwa alikwenda kulalamika kwa Waziri wa Tamisemi juu ya mwenendo wa kiongozi huyo na mvutano uliopo, na kwamba Waziri wa wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) alimtuma Naibu Waziri, Aggrey Mwandri, ambaye alizungumza na viongozi hao kwa kuwaeleza majukumu yao kila mmoja.
Alidai kuwa mara kwa mara Gambo amekuwa akimtukana, kumdhalilisha na kudai kuwa hafai kuwa diwani ikiwa ni pamoja na kudhalilisha watumishi wengine wa halmashauri akiwamo Mwanasheria wa Halmashauri kuwa ana shahada aliyoipata Chuo Kikuu kwa upendeleo.
Alidai kuwa amefanyakazi tangu mwaka 1970 na wakuu wa wilaya zaidi ya 30, lakini hajawahi kukutana na kiongozi wa aina hiyo.
Shahidi wa tatu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Korogwe, Anna Mwalende, alidai kwa miezi mitano alivyofanya kazi na Gambo ilikuwa ni kipindi kigumu kilichojaa manyanyaso ikiwamo watumishi kuswekwa rumande kwa maelekezo yake.
Alidai kuwa utawala wa mabavu, ubabe na lugha chafu umekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya halmashauri na mara kwa mara amekuwa akiitisha vikao vya kamati ya ulinzi na usalama kwa simu badala ya kutumia barua.
Alidai kwa mazingira hayo imetokea mara kadhaa ameshajiandaa kwa vikao muhimu vya halmashauri na wakati huo huo mkuu huyo wa wilaya amepiga simu ya kuwaita na anayotumia mwakilishi humkataa.
”Ilifika mahali mimi na DC hatuongei na hata kwenye vikao, nililazimika kukaa kimya, alituita ofisini kwake mimi, Afisa Utumishi na Afisa Elimu, akitushinikiza kuirejesha kazini mwalimu aliyekuwa ameondoka wa kwenye orodha ya malipo, tulivyokataa aliagiza tukamatwe na kuswekwa ndani, nilikataa, lakini Afisa Utumishi alikamatwa na kuswekwa rumande,” alisema.
Alidai kuwa Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani, ndiye aliyeenda kumuwekea dhamana mtumishi huyo na kwamba alipoamia (DED) kwenye halmashauri hiyo alikuta maelekezo ya kumchukulia hatua mtendaji wa mji wa Mombo, na alivyotaka kutekeleza maelekezo hayo, mkuu huyo wa wilaya ailingilia kati kushinikiza asichukuliwe hatua.
Mwahalende alidai kuwa kutokana na shinikizo la mkuu huyo, miradi miwili imeshindwa kutekelezwa ambayo ni uuzwaji wa viwanja vya mji mdogo wa Mombo ambao ungeipatia Halmashauri kiasi cha Sh. milioni 200 pamoja na mradi wa maji.
Alidai kwa miaka 24 ya utumishi wake, saba ya serikali kuu na 14 katika halmashauri za wilaya amefanyakazi na viongozi wengi lakini kwa kipindi cha miezi mitano hajawahi kukutana na suluba za kiongozi huyo.
Shauri hilo liliahirishwa hadi kikao kingine ili kutoa nafasi kwa shahidi Mwahalende kuwasilisha ushahidi wake wa maandishi.
Madiwani wengine waliofikishwa mbele ya Baraza hilo ni Ulole Juma, Diwani wa Kata ya Kijitonyama, Dar es Salaam ambaye anadaiwa kutotoa tamko la mali na madeni kwa kipindi cha miaka minne ambaye katika maelezo yake alidai kipindi chote udiwani wake ulitenguliwa kutokana na kesi iliyokuwapo mahakamani.
Diwani mwingine ni wa kata ya Kunduchi, Dar es Salaam Rite, ambaye haikutoa tamko hilo kwa miaka ya 2012/13, ambaye alidai alijaza na kufikisha ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na kushangazwa kwa fomu hizo kutofikishwa.
Diwani wa kata ya Magomeni, Juliani Bujugo, alidaiwa hajawasilisha fomu za miaka ya 2011/13, ambaye katika utetezi wake alidai kuwa ni kutokana na kuuguliwa kwa mke wake kwa muda mrefu.
Jaji Msumi, alisema watafanya maamuzi na kuyawasilisha sehemu inayohusika.
SOURCE: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment