Mvua iliyonyesha kwa saa mbili katika maeneo mbalimbali ya Jiji
la Dar es Salaam jana, imeleta kero kwa wasafiri wa vyombo vya moto na
watembea kwa miguu na kusababisha baadhi ya barabara kushindwa kupitika
kutokana na kujaa maji.
Mvua hiyo iliyoanza saa nne asubuhi hadi saa sita
mchana, ilisababisha baadhi ya barabara kutopitika ikiwamo ile ya Samora
karibu na Jengo la Wizara ya Nishati na Madini, baadhi ya maeneo ya
Upanga na Msasani.
Aidha, watumiaji wa Barabara za Azikiwe, Bibi Titi
na Morogoro katikati ya jiji walikuwa na wakati mgumu kupita, wengi
walionekana wakiwa wamevua viatu au kutafuta njia mbadala kukwepa maji
hayo ambayo yalionekana kuchanganyika na majitaka yaliyotokana na baadhi
ya chemba kujaa.
Eneo linalojengwa njia za mabasi ya haraka katika
eneo la Akiba, lilifunikwa na maji na kusababisha usumbufu kwa vyombo
vya moto na watembea kwa miguu.
Maeneo ya Kariakoo, Barabara ya Uhuru na Msimbazi,
yalijaa maji kama ilivyokuwa Barabara ya Umoja wa Mataifa na kuelekea
Hospitali ya Taifa Muhimbili ambazo zilikuwa hazipitiki kutokana na mvua
hizo na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.
Wakazi wa mabondeni walianza kuingiwa na hofu ya
kukumbwa na mafuriko wakati hali ya hewa ilipokuwa inabadilika huku mvua
ikiongezeka kwa kasi. Katika bonde la Msimbazi, Kigogo na Jangwani
wakazi walionekana wenye hofu baada ya mvua kuongezeka.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe
alikataa kusema lolote na kusukuma mpira kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya
Ilala, Isaya Mgurumi.
Hata hivyo, Mgurumi alipopigiwa simu yake ya kiganjani ilikuwa inaita bila kupokewa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA), Agnes Kijazi alisema hayo ni matokeo ya taarifa ya hali
ya hewa waliyoitoa Oktoba, Novemba na Desemba ambayo yalibainisha kuwa
kutakuwa na vipindi virefu vya jua katika msimu wa mvua pamoja na mvua
kubwa. Alisema mvua zilizonyesha jana, zinanyesha mwisho wa msimu wa
mvua kama ilivyotabiriwa kabla.
Kijazi alisema kesho (leo) wanatarajia pia mvua
kubwa kutokana na kuwapo kwa mkandamizo mkubwa wa hewa katika pwani ya
Madagascar.
“Kesho (leo) tutatoa taarifa nyingine ya hali ya
hewa kwa kipindi cha miezi mitatu mingine, hivyo wananchi watumie
taarifa hiyo katika mipango yao mbalimbali,” alisema mkurugenzi huyo.
Wakazi walonga
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, wakazi wa
mitaa hiyo walisema hali hiyo ya chemba kufurika imeshakuwa sugu na
hakuna mikakati thabiti wa kukabiliana na tatizo linapotokea.
Dereva taksi katika Mtaa wa Azikiwe, Frank
Emmanuel alisema jiji linatoa harufu ya majitaka, hususan kuanzia Jengo
la Benjamin Mkapa hadi kituo cha mafuta katika makutano ya barabara za
Upanga na Azikiwe. “Eti ndiyo wanasema mjini hapa! Mvua imenyesha kidogo
maji haya ya kinyesi yamejaa na kuleta adha kwa wananachi… hii ni
hatari kwa afya zetu.”
Mkazi mwingine, Mustafa Said alizitupia lawama
mamlaka husika kwa kushindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo akisema hali
hiyo imekuwa ikijirudia mara kwa mara wakati wa mvua.
“Mvua hii ikiacha kunyesha na wakishaona na kusoma
katika vyombo vya habari kesho watakuja kufanya matengenezo lakini
baada ya muda mfupi mambo ni yaleyale,” alisema Said.
Mkazi mwingine, Josephine Joseph aliitaka Manispaa
ya Ilala kulishughulikia suala hilo ambalo alisema limekuwa kero
hususan maeneo ya Akiba katika makutano ya Barabara ya Morogoro na Bibi
Titi kwani mara kwa mara mvua inaponyesha maji hujaa.
“Wakati mvua ikiendelea kunyesha hapa magari
hayawezi kupita, maji haya yenye kinyesi yalijaa hadi kule upande wa
pili. Tunaiomba manispaa ishughulikie kero hii,” alisema akiwa katika
kituo cha CBE akisubiri usafiri kwenda Mwananyamala.
Alichowahi kusema RC
Desemba 16, mwaka huu wakati akifungua kikao cha
kwanza cha wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa
Mkoa huo, Said Mecky Sadiki aliwataka wahandisi wanaosimamia ujenzi wa
miradi ya barabara katika jiji hilo kuhakikisha wanawasimamia ipasavyo
makandarasi wanaojenga miradi hiyo ili ikamilike kwa viwango na muda
uliopangwa na kuwaondolea wananchi adha ya usafiri na barabara kujaa
maji nyakati za mvua.
Katika kukabiliana na changamoto za miundombinu ya
barabara katika Jiji la Dar es Salaam, zaidi ya Sh88 bilioni
zilipendekezwa kuidhinishwa katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 kwa lengo
la kufanya ukarabati wa kawaida, matengenezo ya barabara za zamani na
mpya kwa kiwango cha lami na ujenzi wa madaraja mapya na yale
yaliyoharibiwa wakati wa msimu uliopita wa mvua.
Alizitaka mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali
vya ujenzi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam,
kuwachukulia hatua za kisheria wananchi wanaovunja sheria kwa kujenga
majengo na kuta katika maeneo yasiyoruhusiwa na kuziba mifereji ya maji
na kubomoa kingo za mito hali inayosababisha mafuriko katika makazi ya
watu wakati wa msimu wa mvua.
Chanzo;Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment