Ikiwa imebaki miezi 10 tu kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu
mwakani, CCM kinaonekana kuteswa na tuhuma za rushwa inayodaiwa kutolewa
na makada wake wanaotajwa kutaka kuwania nafasi mbalimbali ukiwamo
urais.
Hali hiyo inabainishwa na kauli za baadhi ya
makada wa chama hicho katika ngazi mbalimbali ambao wameamua kulalamika
waziwazi ama kupitia vyombo vya habari au kwenye mitandao ya kijamii.
Moja ya kauli hizo ni ile iliyotolewa juzi na
Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki kwenye akaunti yake ya
Twitter akisema: “Mgawo wa Xmass na Mwaka Mpya kwa wajumbe husika wa CCM
ni kucheza na ugumu wa maisha uliopo. Ni ununuzi wa nafasi na si uwezo
wa uongozi. Aibu.”
Alipotakiwa kufafanua kauli yake, Kagasheki
alisema kwenye maoni yake hakutaja mtu licha ya kwamba wapo wengi
wanaotoa zawadi, lakini baada ya kuandika katika mtandao ameandamwa na
baadhi ya watu huku wengine wakimtolea lugha chafu.
“Hii ni line yangu ninaitumia kutoa mawazo siku
zote, lakini nimeshangaa leo watu wameshikia kidedea maoni hayo mpaka
wengine wanatumia lugha kali... sijamtaja mtu kwa sababu najua wapo watu
wengi wanaotoa zawadi,” alisema Balozi Kagasheki aliyewahi kuwa Waziri
wa Maliasili na Utalii huku akisisitiza kuwa hayo ni mawazo huru ambayo
anayaamini.
Waliyonena kuhusu rushwa
Kauli ya Kagasheki haina tofauti na zile
zilizowahi kutolewa na makada wengine, akiwamo mwenyekiti wake, Rais
Jakaya Kikwete na wengine waliowahi kushika nyadhifa za juu ndani ya
chama hicho na Serikali yake juu ya kukithiri kwa rushwa katika kusaka
madaraka.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula
alimwambia mwandishi wetu jana kuwa suala hilo linafuatiliwa kwa karibu
na dawa yake itaiva Februari baada ya kamati yake ya maadili
iliyofuatilia kutoa tathmini yake.
“Tulipotangaza kuwafungia, tuliunda kamati ya
ufuatiliaji harakati za kila mmoja kuona je, yale tuliyomtaka
kutoyafanya ametekeleza? Sisi tunaheshimu vikao vyetu, hivyo tunasubiri
kamati hiyo itakapotuletea taarifa yake.
“Katika tathmini hiyo kama watakuwapo wa kusamehewa watasamehewa na kama watakuwapo wa kuongezewa adhabu wataongezewa.”
Kauli ya Mangula ilikuwa inafafanua makada wa
chama hicho waliopewa onyo kali kwa kufanya kampeni mapema na
kujihusisha na vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na ndani ya
jamii.
Mangula alisema hayo wakati kukiwa na madai kuwa
baadhi ya wanachama wake kudaiwa kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano
mkuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) Zanzibar na maeneo mengine ya
nchi.
Mangula jana alikaririwa na gazeti la CCM, Uhuru, akijibu madai
hayo kuwa, “hakuna mwanachama aliye juu ya katiba, kanuni na miongozo ya
chama na hivyo hakitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kutumia fedha.”
Kwa mujibu wa madai hayo, kada mmoja wa CCM
anadaiwa kugawa kati ya Sh1 milioni na Sh500,000 kama zawadi ya sikukuu
ya Krismasi kwa wajumbe wa vikao vya chama visiwani humo.
Mangula alisema kutokana na malalamiko hayo, CCM
itapeleka timu ya uchunguzi kupitia kitengo cha usalama na maadili
kuchunguza tuhuma hizo.
Oktoba 25, mwaka jana Rais Kikwete alisema endapo
rushwa haitakomeshwa ndani ya CCM, kitaanguka vibaya katika Uchaguzi
Mkuu 2015 na iwapo kitanusurika hakitapita mwaka 2020.
Kauli hiyo pia inaungwa mkono na Waziri Mkuu
mstaafu, Frederick Sumaye aliyewahi kuliambia gazeti hili kuwa iwapo
misingi ya uchaguzi ndani ya CCM itaendelea kulalia kwenye rushwa,
hataendelea kuwa sehemu yake na kuonya kuwa tatizo hilo limefikia pabaya
na litakiangusha chama hicho.
Mwaka 2011, Rais Kikwete alitangaza mkakati wa
‘kujivua gamba’ akiwataka makada wa chama hicho wanaotuhumiwa kwa
ufisadi kutafakari na kujiondoa ndani ya siku 90, lakini hata baada ya
muda huo kumalizika, mkakati huo uliyeyuka na viongozi wakaanza kubadili
maudhui yake.
Waliopigwa ‘stop’
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira,
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na
aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Wanavyoitazama CCM
Wachambuzi waliozungumza na gazeti hili walisema
CCM hakiwezi kupambana na rushwa kwa sababu baadhi ya viongozi wake ni
walarushwa na wamekiondoa katika misingi ya kuwatumikia wananchi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM),
Bashiru Ally alisema: “Chama hakiongozwi kwa makaripio, mkakati wa
kujivua gamba na matamko katika vyombo vya habari. Kinaongozwa kwa
mifumo imara, fikra sahihi, dira na historia yake nzuri.
“Ndiyo maana wanachama wa CCM wamekuwa wakitenda
mambo kinyume na katiba ya chama chao na hakuna wa kuwachukulia hatua.
Kolimba (marehemu) aliwahi kusema kuwa CCM haina dira wala mwelekeo.
Hilo linaonekana sasa, kimeshindwa kukemea rushwa.”
Alisema ni vigumu kwa CCM kuikataa rushwa wakati baadhi ya
wanachama wake, tena wenye nyadhifa za juu ndani ya chama hicho
wakituhumiwa kwa rushwa.
“Mchawi yupo ndani ya CCM yenyewe. Profesa
Tibaijuka ni mjumbe wa Kamati Kuu na amepewa mgawo wa escrow lakini
chama kipo kimya. Jimbo la Bukoba Vijijini limegawanyika kwa sababu ya
rushwa inayotolewa na wanaotaka ubunge, hayo yote CCM hawayaoni na
kukimbilia yanayotokea Zanzibar,” alisema. Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo
Kikuu Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema: “CCM ni chama ambacho
kinajibu mapigo ila hakitoi mapigo. Kinachotokea sasa ni dalili mbaya
kwake kwani kimekuwa dhaifu katika kuwashughulikia wanachama wake wasio
waadilifu.”
Alisema matamko mengi ya chama hicho ni ya kisiasa
zaidi na mengi huishia katika vyombo vya habari. “Hayo yanamaanisha
kuwa uwezo wa CCM umepungua. Mfano ni Chadema kwa sasa kinatoa mapigo na
si kujibu mapigo pekee. Hiyo ndiyo inatakiwa kufanywa na chama cha
siasa,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema
Mangula alipotangazwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM aliahidi kupambana
na rushwa na mpaka leo kashindwa
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment