Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu, amesema serikali itaendelea
kuboresha uhusiano wake na viongozi wa dini katika kupambana na wimbi la
vitendo vya ujangili nchini.
Akizungumza katika mkutano na viongozi hao jijini Dar es Salaam
jana, Nyarandu alisema ongezeko hilo limesababisha madhara makubwa kwa
serikali kupoteza rasilimali za wanyama ambayo ni tegemeo kwa mapato.
Alisema kundi la majangili limeingia katika mbuga mbalimbali za
wanyama kama Tarangire, Manyara, Mikumi, Ngorongoro na kusababisha idadi
kubwa ya wanyama kuuliwa bila sababu.
Alisema viongozi hao wana nafasi kubwa ya kufichua kundi hilo la
majangili kupitia nyumba za ibada yakiwamo na maeneo mengine ya shughuli
za kijamii.
Kadhalika, aliwataka viongozi hao kuweka agano la pamoja katika
kutatua changamoto hiyo hasa kwa kukubaliana ni jinsi gani ya kuzilinda
rasiliamali hizo.
“Tunachofanya ni kuweka mpango madhubuti endelevu ila jukumu kubwa
litakuwa kwa viongozi wa dini, kwa sababu wao wanakutana na watu wengi
kwa nyanja mbalimbali tofauti na serikali,” alisema Nyarandu.
Alisema ili kukabiliana na ongezeko hilo, wizara yake imeongeza
kikosi cha askari wa wanyamapori kitakachodhibiti majangili mara na
baada ya kufanya uhalifu.
Pia, aliwashauri waweke mfumo endelevu kwa kushirikiana na serikali
kwa pamoja kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto hiyo, ingawa ni
kubwa kuliko serikali inavyodhani.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino
Mokiwa, alisema kutokana na mtandao wa ujangili kukua kwa kasi nchini,
huku ukiongoza kuwa mstari wa mbele kuchangia nyumba za ibada, ni jukumu
la viongozi kuwa makini na jambo hilo maana ni dhambi mbele za Mungu.
“Nafikiri katika hili hata sisi viongozi wa dini tunahusika
kushtakiwa mbele za Mungu, kwa sababu tumekuwa tukiwapa kipaumbele
katika nyumba za ibada kwa kisingizio cha kutoangalia matendo yake bali
michango yao,” alisema Askofu Mokiwa.
Aliishairi serikali kutoa adhabu kwa majangili inayofanana na ile
ya mauaji mengine kwani kitendo hicho ni ishara mbaya mbele za Mungu.
“Kumuua mnyama ni dhambi kama dhambi nyingine, hivyo tunapendekeza
adhabu zao ziangaliwe kuanzia shina, kiungo na msambazaji,” alisema.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, aliwataka
Watanzania kuwathamini wanyama kama viumbe vingine vilivyoumbwa na
Mungu.
Alisema Watanzania wengi wamekuwa wakipotoshwa na waganga wa
kienyeji kwa kuwatumia wanyama pori hasa kwa vitendo vya kikatili kama
sehemu ya kafara kwa mihadi mbalimbali ya maradaka na kwamba
usafirishaji wake hadi uuaji wake ni wa kikatili.
“Mungu ameruhusu mnyama auliwe kwa sababu maalum, hivyo kuwatumia
au kuwaua wanyama kinyume cha maandiko ya Mungu ni dhambi,” alisema
Sheikh_ Salum.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment