Mkurugenzi
Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akitoa ufafanuzi kwa
waandishi wa habari kuhusu ujio wa sheria mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 iliyopitishwa na Bunge Mwezi
Machi mwaka huu leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi wa Takwimu za
Uchumi wa Ofisi hiyo Bw. Morrice Oyuke
Ofisi ya Taifa ya
Takwimu imesema kuwa Sheria Mpya ya Takwimu ya mwaka 2015 haina lengo la kuzuia
Taasisi au watu binafsi kufanya tafiti zao hapa nchini bali inalenga kuweka
misingi imara ya shughuli za kitakwimu na tafiti zenye ulinganifu unaotokana na
mfumo rasmi utakaoondoa uwepo wa takwimu
zinazokinzana.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam
na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati akitoa
ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu ujio wa sheria hiyo mpya iliyoridhiwa
na Bunge Mwezi Machi mwaka huu.
Amesema kuanzishwa kwa sheria
hiyo kunalenga kutoa mwongozo kwa Taasisi za Serikali na Mashirika mbalimbali
yanayozalisha takwimu hapa nchini ili yaweze kuendesha shughuli za ukusanyaji
na usambazaji wa takwimu kwa kuzingatia sheria hiyo mpya na kuwa huru kutoa
takwimu sahihi zinazoendana na uhalisia
wa Tanzania.
“Sheria hii hailengi
kuondoa uhuru wa taasisi nyingine za utafiti za
utafiti zilizopo kisheria kufanya kazi zao, taasisi hizo zitaendelea kuwa huru kufuata taratibu zao ilimradi hazikiuki sheria hii” Amesisitiza Dkt.Chuwa.
Amefafanua kuwa kifungu
cha 20 cha sheria hiyo,kinaeleza kuwa takwimu zinazotolewa na taasisi zilizo nje ya
Serikali lazima zikidhi vigezo vya kitakwimu vilivyowekwa na NBS ili ziweze kutumika kupanga mipango ya maendeleo.
Kuhusu wanafunzi wa vyuo
vikuu wanaofanya tafiti mbalimbali chini ya wahadhiri wa vyuo vikuu Dkt. Chuwa amesema ipo
sheria inayowalinda na kusimamia matokeo ya tafiti zao zinazosambazwa kwa
utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha vyuo vikuu.
Ameongeza kuwa sheria hiyo katika kifungu cha 37
(3) imeainisha makosa mbalimbali na adhabu ya kifungo kisichopungua miezi 6 au faini isiyopungua shilingi milioni moja.
Ameyataja makosa hayo kuwa ni upotoshaji
wa ukweli kuhusu takwimu rasmi utakaofanywa na vyombo vya habari, vitendo vya
kuzuia msimamizi, mdadisi au karani wa Sensa kutekeleza majukumu yake
kisheria,kukataa kwa makusudi kujaza fomu au nyaraka yoyote au kujibu maswali
yaliyoulizwa, kutoa taarifa zisizo sahihi, kuharibu fomu au nyaraka yoyote na mtu yeyote kujifanya msimamizi , mdadisi au
karani wa Sensa kwa lengo la kupata taarifa ambazo hastahili kuzipata.
Makosa mengine ni yale
ya kushawishi mtu asishiriki katika zoezi la kitaifa Kitakwimu litakaloendeshwa na
Ofisi hiyo kwa mujibu wa sheria hiyo, kukataa kutoa
nyaraka zozote zinazohitajika katika shughuli za kitakwimu na kukiuka kifungu
chochote cha sheria hiyo.
Kuhusu mchakato wa kupatikana
kwa sheria hiyo amesema umezingatia vigezo vyote ikiwemo Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha muswaada wa
Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 katika Mkutano wake wa 19 na kisha kujadiliwa
Bungeni, Muswaada huo kuwasilishwa kwa wadau ambao waliujadili na kutoa
maoni ambayo yalisaidia kuboresha muswaada huo.
Amesema kuwa kutakuwa na kamati maalumu ya kitaalam itakayoundwa kwa ajili ya
kuangalia takwimu zitakazokuwa zinakusanywa ili kuhakikisha kuwa hakuna ukiritimba wowote unaojitokeza katika kuthibitisha
na kupitisha tafiti na takwimu zitakazowasilishwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Amesisitiza kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea kutoa elimu kwa
umma ikiwemo kuzumgumza na vyombo vya habari ili kujenga uelewa wa umuhimu wa
sheria hiyo kwa maendeleo ya Taifa.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment