Immaculate Makilika na Abushehe Nondo
MAELEZO
Dar es Salaam.
8.9.2016
WAKUU
wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kutumia kipindi
cha miezi 3 hadi Januari mwakani ili kuupitia upya mkataba wa mahusiano
ya kiuchumi na kibiashara kati ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na
Ulaya (EPA) kabla ya kukubaliana na baadhi ya vipengele vya mkataba
huo.
Akizungumza
katika mkutano wa 17 wa Jumuiya hiyo leo Jijini Dar es Salaam,
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. John Pombe Magufuli alisema hatua hiyo imetokana na mjadala na
majadiliano ya kina kutoka kwa Wakuu wa Jumuiya hiyo.
Rais
Magufuli alisema kwa mujibu wa mkataba huo, Umoja wa Ulaya ulitaka
mkataba huo usainiwe mwaka huu, ambapo hata hivyo kwa kuzingatia maslahi
na ustawi wa jumuiya hiyo, Viongozi wa nchi wanachama wamehitaji muda
zaidi wa kufanya maamuzi juu ya mkataba huo.
Dkt. Magufuli alisema kufuatia uamuzi huo, Viongozi hao wameitaka
Sekretarieti ya Jumuiya hiyo kuandaa utaratibu wa kusimamia masuala ya
mahusiano kuhusu mkataba huo kwa kufanya mawasiliano na Umoja wa Ulaya.
“Tumewaomba
wenzetu wa Umoja wa Ulaya wasiiadhibu nchi ya Kenya kwa kuwashinikiza
kusaini mkataba wa EPA ifikapo oktoba mosi mwaka huu, ni vyema nchi zote
wanachama tujiridhishe na vipengele vya mkataba huo kabla ya kuweka
saini ya makubaliano” alisema Rais Magufuli.
Akitolea mfano baadhi ya sababu zinazoifanya
nchi za Jumuiya hiyo kuhitaji muda zaidi wa majadiliano kuhusu mkataba
huo ni pamoja na uhakika wa kulinda viwanda vya ndani vya nchi
wanachama, njia bora za kulinda maslahi ya wakulima, namna bora ya
makusanyo ya kodi za bidhaa kutoka nchi za Ulaya.
Kwa
upande wake, Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema katika ulimwengu wa
sasa suala la utengamano wa jumuiya unahitaji zaidi wingi wa watu na
uwezo wa kujitosheleza kwa uzalishaji na masoko yatakayoyosaidia ukuaji
wa uchumi kwa nchi wanachama.
“Mwaka
1960 idadi ya watu katika nchi za Afrika Mashariki ilikuwa na takribani
watu Milioni 40 ukilinganisha na watu Milioni 165 waliopo sasa ambapo
uwezo wa uzalishaji na masoko umeongezeka, hivyo hatuna budi kuwa na
jumuiya yenye uwezo wa kuzalisha bidhaa kwa wingi na kutoa huduma” alisema Museveni.
Aidha
Museveni aliutaka Umoja wa Ulaya kukubaliana na uamuzi wa wakuu wa
jumuiya hiyo kuwapa muda zaidi wa kufanya maamuzi kuhusu mkataba huo
ambao umebeba maslahi mapana zaidi kwa wananchi wa jumuiya.
Naye
Naibu Rais wa Kenya, William Ruto alisema maamuzi kuhusu mkataba huo
yanalenga usawa na kuimarisha umoja baina ya nchi wanachama hivyo ili
dhana hiyo iweze kwa wananchi ni wajibu wa Viongozi kuweka maslahi ya
wananchi wao.
Aidha
katika mkutano huo, Wakuu wa Jumuiya hiyo walipokea ripoti mbalimbali
ikiwemo ripoti ya mgogoro wa Burundi, ripoti ya mabaraza la mawaziri wa
jumuiya hiyo kuhusu hali ya kisiasa inayoendelea nchini Sudan Kusini
pamoja na uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo.
0 comments:
Post a Comment