Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Rais
wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba amekana kuhusika na
utumaji wa ujumbe katika mitandao ya kijamii juu ya kuitisha mkutano na
waandishi wa habari.
Kauli
hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Rais wa Shirikisho hilo
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya ujumbe huo uliokuwa
ukisambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kumuhusisha Rais wa
Shirikisho hilo.
Mwakifamba amesema kuwa ujumbe huo umeeleza kuwa Rais wa shirikisho hilo atakuwa na mkutano na
waandishi wa habari utakaohusu wasanii waliokipigia kampeni Chama cha
Mapinduzi (CCM) na kutolipwa fedha zao pamoja na kuunga mkono jitihada
za msanii Wema Sepetu kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA).
“Kiukweli sikushiriki kwa namna yoyote katika kuuandika ujumbe
huo na nimesikitishwa kuona kwamba huo ujumbe unasambazwa ukiwa na jina
langu hivyo umeniletea picha mbaya kwani ni kinyume na taratibu na
sheria za Shirikisho,”alisema Mwakifamba.
Amefafanua
kuwa Shirikisho hilo sio chama cha siasa na hawajasajiliwa na msajili
wa vyama vya siasa bali wamejisajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) na kazi zote zinafanyika kwa Sheria Na. 4 ya mwaka 1976 ambayo
iko chini ya Bodi ya Filamu Tanzania.
Ameongeza
kuwa mwanachama wa shirikisho hilo hafungwi kuwa mwanachama wa chama
chochote cha siasa lakini kwa mujibu wa katiba ya vyama na shirikisho ni
marufuku siasa kuletwa katika shirikisho au vyama vyake.
Kwa
upande wake Afisa Mipango wa Chama cha Waigizaji, Saimon Mwapagaja
ametoa rai kwa wananchi wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa lengo
la kuchafua majina ya watu kuacha tabia hiyo kwani inashusha hadhi ya
mtu husika na sio utaratibu mzuri.
“Changamoto
tulizonazo katika tasnia ya filamu ni nyingi sana hivyo ifike wakati
wasanii tuanze kuangalia vitu vya msingi na vyenye tija vitakavyomaliza
changamoto hizo, pia wananchi wapunguze kujiamulia kufanya mambo ambayo
baadae yanaweza kumsababishia muhusika matatizo mabukwa,” alisema
Mwapagaja.
0 comments:
Post a Comment