JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri wa Mambo ya Nje wa
Norway kuzuru Tanzania
Waziri wa Mambo ya Nje wa
Ufalme wa Norway, Mhe. Borge Brende atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili
nchini tarehe 29 na 30 Juni 2017. Madhumuni ya ziara ya Mhe. Brende ambaye
atawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 29 saa tatu usiku ni kuimarisha mahusiano kati
ya Norway na Tanzania.
Wakati wa ziara yake, Mhe.
Waziri Brende pamoja na mambo mengine atafanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Ikulu jijini Dar es
Salaam tarehe 30 Juni 2017.
Aidha, siku hiyo hiyo
asubuhi, mgeni huyo atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Mhe. Dkt. Augustine
Mahiga (Mb.) kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere na
baadaye wataweka saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kuhusu Ushirikiano wa
Mashauriano ya Kisiasa na Kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Mhe. Borge pia atakutana
na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Philip Mpango (Mb.) ambapo kwa pamoja watashiriki
katika uzinduzi wa programu ya kushirikiana katika masuala ya kodi na uzinduzi
wa awamu ya pili ya programu ya kuendeleza mafuta(oil for development program)
utakaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro tarehe 30 Juni 2017. Uzinduzi wa programu hizo pia utahudhuriwa na
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb.) na Kamishna
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Dkt. Charles Kichere.
Ratiba ya ziara ya Waziri
wa Mambo ya Nje wa Norway inaonesha pia kwa kushirikiana na Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb.) na Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani watashiriki katika shughuli za kufunga semina
ya Mradi wa Kusindika Gesi asilia (LNG) iliyoandaliwa na kampuni ya mafuta ya kutoka
Norway inayoitwa Statoil ambayo pia inaendesha shughuli zake hapa nchini. Semina
hiyo inafanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Mhe. Waziri baada ya
kukamilisha ratiba yake nchini atarejea Norway siku ya Ijumaa tarehe 30 Juni
2017 saa nne usiku.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 29 Juni 2017
0 comments:
Post a Comment