Imeandikwa na Shadrack Sagati
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza mkakati wa kuwapiga msasa
wafanyabiashara kutoka China ili watambue kodi wanazotakiwa kulipa
serikalini na taratibu wanazotakiwa kufuata wakati wanapokuwa wanaishi
nchini.
Kwa kuanzia jana, TRA ilianza kuwaelimisha wafanyabiashara wa China,
wanaofanya kazi katika wilaya ya Ilala, ambao mamlaka hiyo ilikiri kuwa
wamekuwa hawafuati taratibu kadhaa za kulipa kodi.
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano na wilaya ya Ilala na idara
ya uhamiaji. Meneja wa Elimu kwa Walipa Kodi wa TRA, Diana Masalla
alisema jana kuwa maeneo ambayo wanawaelimisha wafanyabiashara hao wa
China ni ulipaji wa kodi ya mapato, ulipaji wa kodi ya ufundi stadi,
ulipaji wa kodi wanayokatwa wafanyakazi (PAYEE) na matumizi ya mashine
za malipo za kielektroniki (EFDs).
Masalla alisema pia kwenye semina hiyo, watawaelimisha
wafanyabiashara namna ya kuandaa hesabu za biashara, kiasi cha kodi
kinacholipiwa kodi kwenye biashara na taratibu zingine za kodi.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, Sophia Mjema alisema
baada ya kuwasajili wamachinga katika wilaya yake ili wachangie kodi
serikalini, sasa wameanzisha mkakati kuhakikisha kuwa wafanyabiashara
kutoka China wanalipa kodi stahiki serikalini.
Alisema katika semina hiyo, watawaelimisha taratibu za kupata vibali
vya kuishi nchini na kufanya kazi nchini, namna ya kulipa kodi kwa
biashara wanayofanya na wafuate taratibu zingine za nchi ili wasiingie
kwenye matatizo.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment