Imeandikwa na Fransisca Emmanuel
MSANII wa fi lamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ atapaswa kutumikia
theluthi ya kifungo chake ambacho ni miezi mitano gerezani kabla ya
mchakato wa rufaa dhidi ya kifungo chake.
Lulu alianza kutumikia kifungo cha miaka miwili juzi baada ya
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumtia hatiani kwa kumuua bila ya
kukusudia msanii Steven Kanumba. Akitoa ufafanuzi wa kisheria katika
mtandao wa kijamii wa Instagram, Wakili wa Lulu, Peter Kibatala alieleza
hakuna cha kufanya kwa Lulu kabla ya kutumikia theluthi ya kifungo
chake.
Alisema kisheria katika miezi hiyo mitano ya kutumikia kifungo,
wanaweza kuomba dhamana wakati wakisubiria rufaa na kama Lulu atakuwa na
bahati anaweza kupata wakati wowote.
Kibatala alisema wanakata rufaa kwa kuwa hawawezi kumuacha kijana wa
miaka 22 mwenye malengo mengi ya baadaye kuyaharibu kutokana na hukumu
za makosa ya jinai. ‘’Dhamana wakati wa kusubiri rufaa isikilizwe pamoja
na kifungo cha nje vinaweza kufanyika wakati mmoja,’’ alisema Wakili
Kibatala.
Wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole alisema sheria ya makosa ya
jinai inasema adhabu ya juu kwa mashitaka ya kuua bila kukusudia ni
kifungo cha maisha lakini hakuna ukomo wa adhabu ya chini.
Kambole alisema mahakama inaweza kutoa adhabu ndogo kutokana na
kigezo cha umri, muda wa kukaa gerezani kwa mshitakiwa na kama ni
mkosaji wa kwanza na kajutia kosa.
‘’Mahakama ndiyo inayoamua kutoa adhabu kwa kuwa sheria inaonesha
adhabu ya juu ni kifungo cha maisha lakini hakuna ukomo wa adhabu ya
chini hivyo inaweza kumhukumu kifungo cha nje, kifungo cha miaka miwili
au mmoja kulingana na sababu hizo,’’ alisema Kambole.
Pia alisema mfano mzuri ni kesi ya mauaji ya bila kukusudia iliyokuwa
ikimkabili askari Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), namba G
58 Pacificius Simon (27) kwa kosa la kumuua bila kukusudia mwandishi wa
habari, Daudi Mwangosi mwaka 2012 kijiji cha Nyololo wilaya ya Mufindi
mkoani Iringa Alisema katika hukumu hiyo, Mahakama Kuu Kanda ya Iringa
ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 15 jela, hivyo
inategemeana na utashi wa jaji, ushahidi na vigezo hivyo.
Mwananchi Tumsifu Mwamini aliwataka wanaotaka kumsaidia Lulu watumie
njia ya sheria kwa kuwa ina msamaha na huruma ndani yake na ni mfumo
ulioruhusiwa na Mungu.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment