WAKATI Rais John Magufuli jana akitimiza miaka miwili tangu aingie
madarakani mwaka 2015, mambo 10 ya msingi ya kimageuzi yametajwa
kutekelezwa chini ya uongozi wake ikiwemo kudhibiti ufi sadi na
kuboresha sekta za afya, elimu na ulinzi wa rasilimali za nchi.
Aidha, imebainishwa kuwa katika uongozi wake uliojikita katika
maamuzi magumu yenye mafanikio, amefanikiwa kuokoa kiasi kikubwa cha
fedha kutokana na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha kwa kuwaondoa
takribani watumishi hewa na wengine waliokuwa wameghushi vyeti vya
taaluma 32,000 pamoja na kufuta safari za nje zisizo za lazima.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya
Habari Maelezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi
wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu tathmini ya miaka miwili
ya uongozi wa Dk Magufuli. Dk Abbasi aliwaambia waandishi wa habari
kuwa katika vita dhidi ya ufisadi, Serikali ya awamu ya tano imekuwa
makini kusukuma mageuzi na kuhakikisha fedha inayopatikana inatumika kwa
ajili ya maslahi ya Watanzania na si kuishia katika mifuko ya wachache.
“Na ndiyo maana alianzisha Mahakama ya Mafisadi ambayo inapokea kesi
zake nyingi kutoka Mahakama za chini. Tangu ianze imepokea mashauri
matatu kati ya hayo, mawili yanasikilizwa Dar es Salaam na moja Mtwara.
Kesi 107 bado zipo chini ya Mahakama za chini, lakini zimepokelewa na
Mahakama hiyo ya Mafisadi kuomba dhamana,” alisisitiza.
Alisema pia katika miaka hiyo miwili, Serikali ya awamu ya tano
imefanikiwa kuleta mageuzi katika sekta za elimu, afya, miundombinu na
miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya Standard Gauge na ya nishati
itakayoongeza megawati zaidi ya 300 za umeme. Alisema katika sekta ya
afya, kupitia bajeti ya dawa, Rais Magufuli aliongeza bajeti ya dawa
kutoka Sh bilioni 30 hadi Sh bilioni 231 katika mwaka wake wa kwanza wa
uongozi na hadi kufikia mwaka wake wa pili wa uongozi bajeti hiyo
ilipanda na kufikia Sh bilioni 261.
“Lakini pia hakuishia hapo tu, Rais ameongeza uwekezaji katika sekta
ya afya ambapo hospitali nyingi za Serikali zimenunuliwa vifaa vya
kisasa zikiwemo mashine za figo na CT Scan,” alisema Dk Abbasi. Kuhusu
elimu, alisema kupitia mpango wake wa kutoa elimu bure darasa la kwanza
hadi kidato cha nne, ndani ya miaka hiyo miwili, Serikali inatumia Sh
bilioni 23 kwa mwezi kwa ajili ya kulipia elimu hiyo bure ambayo ni sawa
na zaidi ya Sh bilioni 300 kwa mwaka. Katika elimu ya juu, Dk Abbas
alisema ndani ya miaka miwili, Rais Magufuli amefanikiwa kuongeza fedha
za mikopo ya wanafunzi kutoka Sh bilioni 48 hadi Sh bilioni 427.
“Lakini pia hadi sasa Serikali hii imewekeza kwenye miradi mikubwa ya
maji kwa lengo ya kuhakikisha maji safi na salama yanawafikia wananchi
na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa reli ya
Standard Gauge ambayo hadi sasa tayari tuta la kilometa 100
limeshajengwa,” alizidi kufafanua Msemaji huyo wa Serikali.
Aidha, miradi mingine mikubwa iliyofanikishwa awamu hiyo ni ununuzi
wa ndege sita za Tanzania ambapo tayari ndege mbili, Bombardier
zimeshawasili na hadi Julai mwakani ndege zote zitakuwa zimeshawasili
ikiwemo ndege kubwa kwa ajili ya safari za kimataifa.
Kuhusu miradi ya nishati, Dk Abbasi alisema Serikali imewekeza katika
mradi wa nyongeza wa Kinyerezi I utakaozalisha megawati za umeme 185
ambao tayari ujenzi wake umefikia asilimia 50, huku mradi mwingine wa
Kinyerezi II wenye uwezo wa kuzalisha megawati 250 za umeme ukitarajia
kuanza kuzalisha megawati 30 mapema mwezi ujao.
Alitayataja mafanikio mengine ya Serikali yaliyopatikana ndani ya
miaka hii miwili kuwa ni pamoja na kuweka msukumo kuhakikisha fedha za
Watanzania zinatumika ipasavyo. Alitolea mfano utaratibu ulioanzishwa wa
kuwaondoa watumishi hewa 20,000 kwenye orodha ya mishahara hali
iliyookoa kiasi cha Sh bilioni 238. Kwa watumishi 12,000 waliondolewa
wenye vyeti feki vya taaluma, alisema Sh bilioni 142.9 ziliokolewa.
“Kilio kikubwa cha wananchi ni rushwa na ufisadi. Uchunguzi ulikuwa
haufanyiki na hata unapofanyika hatua hazikuchukuliwi kwa wakati.
Katika miaka hii miwili mambo kadhaa ya kimageuzi yamefanyika,”
alisema. Alisema baada ya kuondolewa kwa watumishi hao hewa na
walioghushi vyeti 32,000 Serikali katika mwaka huu wa fedha imetangaza
ajira mpya 52,000 za sekta mbalimbali ambazo tayari mashirika na taasisi
za umma zimeshaanza mchakato wa ajira. “Lakini pia si hapo tu tayari
akiwa Zanzibar kwenye maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge, Dk
Magufuli alitangaza rasmi nyongeza ya mishahara ya watumishi wa umma
itaanza kulipwa mwezi huu na wote wanaostahili kupandishwa madaraja,”
alisisitiza.
Alisema pia Rais alipunguza matumizi semina na safari zisizo za
lazima ambapo kabla ya safari hizo kupunguzwa kuanzia mwaka 2014/15
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilikuwa
inatumia Sh bilioni 216 kwa ajili ya safari za nje, lakini Serikali ya
sasa tangu ianze 2015 hadi mwaka huu, imetumia Sh bilioni 25 tu.
“Kwa mfano mwaka huu kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa, Tanzania
tulipeleka watu wanne tu waliofanya vizuri wakati miaka ya nyuma
walikuwa wanaenda watu zaidi ya 100. Mimi Mkurugenzi nimesafiri mara
mbili tu nje ya nchi,” alisema Dk Abbasi. Alisema pia ndani ya kipindi
hicho cha miaka mitano, Serikali hiyo imefanikiwa kuanza kutekeleza
safari ya Tanzania kujitegemea kiuchumi kwa kuhimiza Watanzania
wawajibike kwa kufanya kazi zaidi lakini pia kuongeza kasi ya uzalishaji
na ukusanyaji wa mapato.
Alitolea mfano takwimu za mapato yaliyopatikana ndani ya kipindi cha
miaka hiyo miwili kuwa yameongezeka kutoka Sh bilioni 9.9 mwaka 2015
hadi Sh bilioni 14 Juni, 2017. Aidha alisema Serikali ya Dk Mafufuli
tangu iingie madarakani imefanikiwa kutekeleza uhamiaji wa Serikali
mjini Dodoma baada ya miaka 44 tangu wazo hilo lianzishwe. “Sasa hivi
ofisi zote za serikali zimehamia Dodoma, Makamu wa Rais anatarajiwa
kuhamia wakati wowote kuanzia sasa na Rais Magufuli ametangaza kuhamia
Dodoma wakati wowote kuanzia mwakani,” alieleza.
Pamoja na hayo, alibainisha mambo mengine ya mageuzi yaliyofanywa na
Serikali kuwa ni kutunga Sera na Sheria ya kupigania rasilimali za nchi
na kufanikisha makubalino mapya na kampuni ya uchimbaji dhahabu ya
Barrick yatakayokuwa na manufaa kwa Watanzania. “Lakini pia kuanza
kupitiwa kwa mikataba hasa kwenye sekta ya madini kumeanza kuzaa matunda
kwani kwa upande wa almasi sasa uzalishwaji wake umepanda kutoka karati
za almasi 15,000 had 18,000 na kufikia karati 28,000 hadi 32,000,”
alisema Dk Abbas.
Alisema pia Serikali hiyo imefikia azma ya kuijenga Tanzania ya
viwanda ambapo kuna miradi ya kuanzisha viwanda zaidi ya 3,000 kupitia
Kituo cha Uwekezaji (TIC), Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda
Tanzania (NDC) ma kusajiliwa kama kampuni binafsi. Novemba 5, mwaka
2015, Dk Magufuli aliapishwa rasmi kuwa Rais wa tano wa Tanzania na
kuingia Ikulu baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25,
mwaka huo.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment