Waziri
wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla (MB) anatarajiwa kuwa
mgeni rasmi leo Januari 23.2018, kwenye uzinduzi wa Onesho la Chimbuko
la Binadamu Afrika, tukio ambalo litafanyika majira ya saa 11 jioni
katika viunga vya Makumbusho ya Taifa, yaliyopo mtaa wa Shabani Robert,
mkabala na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).
Akizungumza
jana wakati wa utambulisho wa tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho
ya Taifa, Profesa Audax Mabulla alibainisha kuwa, tayari maandalizi ya
onesho hilo yameenda sawa na watu mbalimbali watanatarajiwa kushuhudia
tukio ambalo ni la siku moja wakiwemo viongozi wa Serikali na Mabalozi
waliopo nchini, na watalii wanatarajiwa kuhudhuria.
Profesa
Mabulla alibainisha kuwa, Vioneshwa vyote katika onesho hilo la leo,
vimepatikana hapa Tanzania kutokana na tafiti za kisayansi na
vimehifadhiwa Makumbusho ya Taifa.
“Vioneshwa
hivi ni pamoja na masalia ya zamadamu, zana za mawe na masalia ya
wanyama walioishi takribani tangu miaka milioni 4 iliyopita. Pia zipo
picha za zamadamu na mazingira waliyoishi wakifanya shughuli zao za kila
siku.” alieleza Profesa Mabulla.
Kwa
upande wake Mratibu kwa upande wa Tanzania Dk. Agness Gidna alisema
Onesho limegawanyika katika sehemu kuu nne zikiwemo Makumbusho ya Taifa
la Tanzania ikishirikiana na Ubalozi wa Spain Tanzania.
Hii
ni pamoja na Makumbusho ya Akiolojia ya Madrid, Taasisi ya Chimbuko la
Binadamu (IDEA) Madrid, Chuo Kikuu cha Alcala Madrid na Makumbusho ya
CosmoCaixa Barcelona-Spain huku tamasha zima likidhaminiwa na Kampuni ya
Simenti ya Twiga.
“Tunawashukuru
kampuni ya Twiga Cement kwa kudhamini onesho la Chimbuko la Binadamu
Afrika (The Cradle of Humankind in Africa). Pia kutakuwa na Semina na
onesho hili ni matokeo ya tafiti mbali mbali zinazofanyika bonde la
Olduvai na Laetoli, Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro.” alieleza Dk
Agness.
Aidha
Dk.Agness aliongeza kuwa, Onesho hilo litakuwa katika pande nne ikiwemo
sehemu ya kwanza inahusu ushahidi wa nyayo za zamadamu zilizongunduliwa
huko Laetoli mwaka 1978 na mtafiti Dkt. Mary D. Leakey. Nyayo hizo
ziliachwa na zamadamu anayeiitwa Australopithecus afarensis na ni
ushaidi usiopingika wa zamadamu kutembea wima kwa miguu miwili takribani
miaka milioni 3.6 iliyopia.
Sehemu
ya pili inahusu hadithi ya kusisimua ya kuwa binadamu (Genus Homo)
ambapo kuna masalia ya zamadamu Zinjanthropus au Paranthropus boisei na
Homo habilis, zana za mawe za mwanzo (Oldowan) zilizotumika katika
kujipatia chakula na ushahidi wa kale wa ulaji wa nyama katika historia
ya mabadiliko ya binadamu, takribani miaka million 2 iliyopita.
Sehemu
ya tatu inahusu maisha ya jamii ya Homo erectus. Jamaii hii inafanana
zaidi na binadamu wa sasa kuliko jamii zilizotangulia. Kuna masalia ya
zamadamu Homo erectus, zana za mawe (Acheulian) na ushahidi wa ulaji wa
wanyama wakubwa kama vile tembo na nyati wa zamani takribani miaka
million 1.7 iliyopita.
Sehemu
ya nne inaonesha kipindi cha mwanzo cha binadamu wa sasa (Homo sapiens)
walioanza kutokea hapa Afrika miaka laki 2 iliyopita. Kuna masalia ya
Homo sapiens na zana za mawe za muhula wa kati na muhula wa mwisho.
Mbali
na onesho hilo, pia waandaji hao wa Makumbusho ya Taifa inawakaribisha
watu wote kuhudhuria semina na ufunguzi wa onesho la Chimbuko la
Binadamu Afrika.
Kwa
upande wa Semina ambayo inatarajia kuanzia majira ya saa tisa kamili
itaendeshwa na watafiti wa Kimataifa, akiwemo Prof. Manuel
Dominguez-Rodrigo wa Chuo Kikuu cha Complutense, Spain; Prof. Audax ZP
Mabulla na Dk. Agness Gidna.
0 comments:
Post a Comment