Msanii
wa Filamu nchini Bibi. Wastara Issa (wapili kulia waliokaa chini)
akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake kuhusu maandalizi ya
safari yake ya matibabu kuelekea Mjini Mumbai walipofanya naye
mazungumza leo Jijini Dar es Salaam. Watatu kulia waliokaa ni Katibu
Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo.
Na Genofeva Matemu – WHUSM
Msanii
wa filamu nchini Bibi. Wastara Issa ameendelea kumshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa kuonyesha
moyo wa kuguswa na tatizo linalomsumbua na kuweza kumpatia kiwango cha
shilingi milioni 15 kwa ajili ya matibabu ya mguu pamoja na mgongo.
Bibi.
Wastara ametoa shukrani hizo leo Jijini Dar es Salaam alipokua
akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa awali ilikua aondoke
nchini tarehe 28 mwezi januari mwaka huu kwenda mjini Mumbai kwa ajili
ya matibabu lakini kutokana na baadhi ya mipango kutokaa vizuri safari
hiyo ilisogezwa hadi jumapili tarehe 4 Februari 2018 ambapo anatarajia
kuondoka mida ya jioni na kufika Mumbai mapema alfajiri siku ya jumatatu
ambapo ataanza matibabu siku hiyo hiyo.
Bibi.
Wastara amesema kuwa katika safari hiyo ataongozana na nesi mmoja
kutoka hospitali ya TMJ pamoja na mtu mmoja kutoka katika familia yake
ambapo matibabu yake yatafanyika katika hospitali ya Saifee iliyopo
Mumbai na kutarajia matibabu hayo kuchukua takribani wiki tatu na
zaidi.
Aidha
msanii Wastara Issa ameishukuru wizara inayosimamia tansia ya filamu
kwa kumfariji katika kipindi hiki kigumu anachopitia huku akimshukuru
Waziri mwenye dhamana na tasnia ya filamu nchini, Bodi ya Filamu
Tanzania, Baraza la Sanaa la Taifa pamoja na watanzania wote kwa
kuonyesha upendo wa dhati kwake.
“Asanteni
sana watanzania mmeonyesha moyo wa dhati kwangu kwa muda mrefu sasa,
mmekua pamoja nami tangu kipindi cha matibabu ya Saduki hadi sasa, uzito
wa neno asante kutoka kwangu leo hauwezi kulipa fadhila kwa dua na
michango yenu kwangu, mwenyezi mungu aendelee kuifanya nchi yetu kuwa na
amani na upendo” amesema msanii Wastara Issa
Naye
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amesema kuwa serikali
kupitia bodi ya filamu inashukuru kwa kupata taarifa kamili ya safari
ya msanii Wastari Issa ilipofikia kwani bodi ya filamu inapenda kumuona
Wastara akiwa katika afya nzuri na kurudi katika hali yake ili aweze
kuungana na wanatasnia wenzake kuendeleza tasnia ya filamu nchini.
Bibi.
Fissoo amesema kuwa Watanzania wengi wamekua wakiwasiliana na Wastara
kwa njia mbalimbali, kumchangia na hata kufika kumuona, hivyo serikali
inatambua kuwa msanii Wastara Issa yupo katika maandalizi ya safari
ambapo awali alikua asafiri tarehe 28 mwezi januari mwaka 2018 lakini
kutokana na taratibu za safari kutokukamili kumepelekea safari hiyo
kusogezwa hadi tarehe 4 Februari mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment